Cristiano Ronaldo alifunga magoli manne katika ushindi wa 4-0 wa Al Nassr dhidi ya Al Wehda kwenye Ligi Kuu ya Saudia.
Kwa magoli hayo, Cristiano Ronaldo amefikisha magoli 503 ya ligi akiwa na vilabu vitano katika ligi tano tofauti.
Ronaldo ambaye ametimiza miaka 38 mwishoni mwa wiki ameandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii kuwa ni furaha kwake kuifungia timu yake na kuvuka magali 500 ya ligi.
Mshindi huyo mara tano wa tuzo ya Ballon d’Or alijiunga na Al Nassr Desemba 2022, lakini hakuwa na mwanzo mzuri ambapo alifunga goli moja kwa mkwaju wa penalti katika mechi zake tatu za kwanza za kimashindano kwa klabu hiyo.
Ronaldo aliondoka Manchester United Novemba 2022, akiwa amefunga mabao 103 katika misimu miwili ya klabu hiyo.
Alifunga mara 311 kwenye La Liga akiwa na Real Madrid, akasajili mabao 81 kwenye Serie A akiwa na Juventus na akafanikiwa kufunga magoli matatu katika ligi kuu ya Ureno katika klabu yake ya kwanza ya kulipwa, Sporting Lisbon.
Mabao manne ya Ronaldo yaliihakikishia Al Nassr kurejea kileleni mwa jedwali kwa tofauti ya mabao na wakiwa na mchezo mkononi dhidi ya Al Shabab wanaoshika nafasi ya pili.