Ronaldo akaliwa kooni

0
2390

Sakata la tuhuma za udhalilishaji wa kijinsia lianalomkabili mshindi wa mara tano wa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia Cristiano Ronaldo limeendelea kuchukua sura mpya na sasa linaonekana kuanza kutikisa masuala yake ya kiuchumi.

Kampuni ya utengenezaji wa vifaa vya michezo ya NIKE ya nchini Marekani  ambayo ina mkataba wa matangazo na nyota huyo imesema  kuwa  inalichukulia kwa uzito sakata hilo na italifuatilia hatua kwa hatua mpaka mwisho wake.

Nayo kampuni ya EA SPORTS ambayo pia ina mkataba na nyota huyo wa Juventus imesema kuwa inafuatilia kwa karibu sakata hilo kutokana na mikataba yao kuwataka wachezaji na mabalozi wake kuwa na tabia njema inayoendana na hadhi ya kampuni hiyo.

Mbali na Ronaldo kukanusha tuhuma hizo za udhalilishaji, klabu yake ya Juventus pia imemtetea na kusema kuwa katika miezi ya hivi karibuni ameonekana kama mchezaji bora kabisa na mfano wa kuigwa na kila mmoja ndani ya klabu hiyo.

Katika hatua nyingine Ronaldo ameenguliwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Ureno kinachojiandaa na michezo mbalimbali ya kimataifa ya kalenda ya FIFA ili kupata muda zaidi wa kushughulikia sakata hilo ambalo kwa kiasi kikubwa limetajwa kuvuruga utulivu wake katika soka.