Rekodi mpya michuano ya EURO 2024

0
884

Michuano ya EURO 2024 sasa imefikia hatua ya fainali ambapo Hispania na Uingereza zitakutana Jumapili ijayo Julai 14 kuamua nani anarudi nyumbani na taji.

Hizi ni baadhi ya rekodi nyingi zilizowekwa kwenye michuano hiyo hadi sasa;

  1. Kinda wa Hispania, Lamine Yamal, aliweka historia kwa kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kucheza katika fainali za EURO alipocheza kwa mara ya kwanza katika ushindi wa 3-0 wa Hispania dhidi ya Croatia akiwa na umri wa miaka 16 na siku 338. Kisha akawa mfungaji mdogo zaidi katika fainali hizo kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi ya Ufaransa, siku 24 baadaye.
  2. Katika mechi ya tatu, Manuel Neuer wa Ujerumani alicheza mechi yake ya 18 ya EURO, akivunja rekodi ya awali ya kipa iliyowekwa na Gianluigi Buffon wa Italia (17).
  3. Arda Güler wa Uturuki alikuwa mchezaji mdogo zaidi kufunga kwenye mechi yake ya kwanza ya EURO alipofunga dhidi ya Georgia akiwa na umri wa miaka 19 na siku 114, akivunja rekodi ya awali ya Cristiano Ronaldo kwa siku 14.
  4. Nedim Bajrami aliipa Albania goli la uongozi katika mechi ya ufunguzi ya EURO dhidi ya Italia baada ya sekunde 23, akivunja rekodi ya awali ya goli la mapema zaidi iliyokuwa ikishikiliwa na Dmitri Kirichenko wa Urusi (sekunde 67).
  5. Julian Nagelsmann wa Ujerumani (miaka 36 na siku 327) alikua kocha mdogo zaidi kuiongoza timu katika mashindano ya EURO, akivunja rekodi ya aliyekuwa kocha wa Slovenia, Srečko Katanec kwa siku sita.
  6. Ubelgiji imecheza mechi nane za hatua za mtoano katika fainali za EURO lakini hawajawahi kwenda muda wa ziada katika mechi yoyote kati ya hizo.
  7. Ujerumani iliifunga Scotland 5-1 na kuwa timu ya kwanza kufunga magoli matano katika mechi ya ufunguzi tangu mechi ya kwanza kabisa katika historia ya EURO mwaka 1960, wakati Yugoslavia ilipoifunga Ufaransa 5-4.
  8. Cristiano Ronaldo amekuwa mchezaji wa kwanza kucheza katika mashindano ya EURO mara sita tofauti, mara yake ya kwanza ikiwa mwaka 2004.
  9. Hispania ilikuwa timu ya kwanza kushinda mechi sita katika toleo moja la fainali walipoifunga Ufaransa kwenye nusu fainali.
  10. Ufaransa hawajashinda mechi yao ya mwisho ya kundi katika mashindano makubwa tisa yaliyopita, tangu walipoifunga Togo 2-0 katika Kombe la Dunia la mwaka 2006.