Ratiba za CAF kuendelea kama zilivyopangwa

0
1353

Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limesema litaendelea na ratiba zake za mashindano  kama kawaida,  licha ya kuenea kwa virusi vya corona katika nchi mbalimbali za bara hilo.

Mechi 48 za kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zinatarajiwa kuchezwa katika mataifa 50 mwishoni mwa mwezi huu,  huku fainali za kombe la mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN)  zikitarajiwa kuanza kutimua vumbi kuanzia Aprili nne hadi 25 mwaka huu nchini Cameroon.

Taarifa ya CAF imesema kuwa, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO)  hakuna nchi ya Afrika iliyotangaza maafa makubwa kutokana na virusi vya corona, hivyo wameamua kuendelea na ratiba za mashindano yote kama zilivyopangwa.

CAF imetoa taarifa hiyo katika kipindi hiki ambapo baadhi ya nchi za Afrika ikiwa ni pamoja na Kenya na Rwanda zikiwa zimeishawazuia wanamichezo kutoka katika nchi hizo kusafiri nje ya nchi.

Mpaka sasa virusi vya corona vimeripotiwa katika nchi 12 barani Afrika huku Misri ikitajwa kuathirika zaidi na Algeria imetangaza shughuli zote za kimichezo nchini humo kufanyika bila mashabiki.

Maafisa wa CAF wanatarajiwa kuitembelea Cameroon kati ya Machi 14 na 15  mwaka huu ili kujiridhisha na hali ya ilivyo kabla ya kuanza kwa fainali za CHAN, nchi ambayo ina wagonjwa wawili wa corona.