Kocha mkuu wa kikosi cha Fulham Muitaliano Claudio Ranieri amesema kuwa kocha wa mpito wa klabu ya Manchester United, – Ole Gunnar Solskjaer anafaa kuwa kocha wa kudumu wa klabu hiyo.
Ranieri amesema kwa sasa kocha huyo ameonyesha ana uwezo wa kukiongoza kikosi hicho cha mashetani wekundu kutokana na matokeo mazuri ya timu hiyo tangu alipoteuliwa kuiongoza kwa mpito akichukua nafasi Jose Mourinho aliyetimuliwa mwezi Disemba mwaka 2018.
Tangu achukue mikoba ya kukiongoza kikosi hicho, Solskjaer ameshinda michezo Tisa na kutoa sare kwenye mchezo mmoja tu kati ya michezo Kumi ambayo timu yake imeshuka dimbani.
Hata hivyo Ranieri anaamini timu yake ya Fulham itatibua rekodi hiyo kwa kuitandika Manchester United kwenye mchezo wa ligi kuu ya England utakaochezwa Jumamosi Februari Tisa.
Ranieri amesema kila kitu kina mwisho, na yeye anataka timu yake ndiyo iumalize mfululizo wa matokeo mazuri wa mashetani wekundu hao na anaamini watafanya hivyo kwa kucheza vizuri zaidi yao.