Mwili uliokutwa kwenye mabaki ya ndege iliyombeba mchezaji Emiliano Sala umethibitika kuwa ni wa mchezaji huyo raia wa Argentina.
Polisi wa mji wa Dorset waliokuwa wanaendesha shughuli ya utambuzi wamesema kuwa baada ya kuutoa mwili huo kwenye mabaki ya ndege aina ya Piper Malibu PA-46-310P na kuufanyia uchunguzi wamethibitisha kuwa ni wa mchezaji huyo aliyekuwa akisafiri kutoka Nantes nchini Ufaransa kuelekea Wales alikokuwa amejiunga na timu ya Cardiff City.
Ndege hiyo ilipoteza mawasiliano Januari 21 mwaka huu ikiwa na Sala pamoja na rubani David Ibbotson ambaye mwili wake bado haujapatikana.
Sala alikuwa anaenda kwenye timu yake mpya ya Cardiff, siku mbili tu tangu akamilishe usajili wa kujiunga na timu hiyo akitokea timu ya Nantes ambako alirejea kwenda kuwaaga wachezaji wenzake.
Baada ya kuthibitika kuwa Emiliano Sala amekufa kwenye ajali hiyo ya ndege, klabu ya Cardiff City na baadhi ya wachezaji wa timu mbalimbali wametuma salamu za rambirambi kwa familia ya mchezaji huyo na familia ya soka ulimwenguni kote.