Pambano la Bondia Hassan Mwakyinyo lililopangwa kufanyika nchini Ujerumani limesogezwa mbele kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona.
Akizungumza na waandishi wa habari Msemaji wa Kampuni ya Swahili Flix, Steve Nyerere amesema kwa sasa dunia inapambana na virusi Corona hivyo wameamua kulisogeza mbele pambano hilo ili waungane pamoja kutokomeza maambukizi ya virusi hivyo.
Kwa Upande wake promota wa ngumi za kulipwa, Jay Msangi amesema pambano hilo lingewakutanisha mabondia wakubwa kutoka nchi mbili tofauti lakini kutokana na mlipuko wa virusi hivyo pambano limesogezwa mbele na litatangazwa tena baada ya siku 30.
Bondia Hassan Mwakinyo alitarajiwa ulingoni Machi 21 nchini Ujerumani kupambana na bondia namba moja nchini Ujerumani katika kuwania mkanda wa WBO International.