Mwalimu Kashasha kuzikwa makaburi ya Kinondoni

0
1089

Mwili wa Mwalimu Theogenes Alexander Kashasha utazikwa Jumatatu Agosti 23, 20221 katika makaburi ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam.

Akizungumza na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Msemaji wa familia, Deusi Kashasha ameeleza kuwa mazishi hayo yatatanguliwa na ibada itakayofanyika katika Kanisa la Ufunuo lililopo Buza Kipera.

Mwalimu Kashasha ambaye alizaliwa mwaka 1957 amefariki Agosti 19 katika Hospitali ya Kairuki baada ya kuungua kwa takribani wiki mbili.

“Familia tumeguswa na kuondokewa na ndugu yetu lakini kazi ya Mungu haina makosa. Mazishi ni tarehe 23 Agosti katika makaburi ya Kinondoni na msiba utakuwepo hapa Majimatitu Mbagala,” amesema Deus Kashasha

Waomboezaji mbalimbali wakiwemo waliokuwa wafanyakazi wenzake, jamaa na marafiki wamefika nyumbani kwa marehemu kutoa pole kwa wafiwa.

Ujumbe wa TBC uliofika nyumbani kwa marehemu umeongozwa na Mkurugenzi wa Huduma za Redio, Aisha Dachi, ambaye amesema kuwa wamehuzunishwa sana na kifo hicho kwani bado walihitaji utumishi wa Mwalimu Kashasha.

Pia wadau mbalimbali wa michezo akiwemo Sunday Manara wamezungumza na TBC na kueleza namna walivyoguswa na msiba huo mkubwa na kwamba wataenzi weledi wake na mchango wake katika sekta ya michezo.

Mwalimu Kashasha ameacha mjane na watoto wawili.