Mtendaji Mkuu wa klabu ya Manchester United ya England, Ed Woodward amejiuzulu wadhifa huo, kutokana na kuwa mmoja wa viongozi waliohusika kwenye wazo na utekelezaji wa uanzishwaji wa Ligi Kuu ya Ulaya (European Super League).
Hatua ya kujiuzulu kwa Ed Woodward imekuja kufuatia shinikizo kubwa kutoka kwa mashabiki wa vilabu sita ambavyo ni Arsenal, Chelsea, Liverpool, Manchester City, Manchester United na Tottenham, ambao wameandamana kushinikiza vilabu hivyo visishiriki kwenye ligi hiyo.
Jana Aprili 20, mchezo kati Chelsea na Brighton ambao uliisha kwa sare tasa (0-0) ulilazamika kuchelewa kuanza kwa takriban dakika 40, baada ya mashabiki kufurika nje wa uwanja wa Stamford Brigde, wakishinikiza klabu hiyo kuachana na mpango huo.
Awali, Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Ulaya (UEFA), lilitoa onyo kali kwa Wachezaji ambao wangeshiriki ligi hiyo kuwa hawatopata vibali vya kucheza kwenye timu zao za Taifa kwenye michuano ambayo inasimamiwa na shirikisho hilo.
Ed Woodward ambaye alijiunga na United mwaka 2005, amedumu katika wadhifa huo kwa kipindi cha miaka 8, na amesema kuwa ataachia wadhifa huo mwishoni mwa msimu huu.