Mourinho atetea kufanya vibaya akiwa na Manchester United

0
1234

Aliyekuwa kocha wa Manchester United ya England – jose Mourinho ametetea mwenendo mbovu  wa timu hiyo ilipokuwa nanye ambao ulipelekea kufukuzwa kazi kwenye timu hiyo mwezi Desemba mwaka jana.

Mourinho amesema watu hawajui kinachotokea nyuma ya pazia ndiyo maana wanakosoa kirahisi matokeo ya kinachofanyika nyuma ya pazia.

Kocha huyo Mreno anasema mambo hayakuwa shwari ndani ya Manchester United ndiyo mana alivurunda kwenye msimu wake wa mwisho hali iliyosababishwa na kutoungwa mkono na bodi ya klabu hiyo.

Anasema kuna maamuzi alikuwa anataka yachukuliwe ili timu ikae sawa lakini bodi haikuonyesha ushirikiano jambao lililopelekea mpasuko kwenye timu na kuifanya ikose matokeo mazuri.

Kati ya mambo ambayo Mourinho amewahi kuyalalamikia hadharani alipokuwa akiwanoa Mashetani Wekundu ni pamoja na uongozi kushindwa kukamilisha usajili wa wachezaji aliokuwa anawataka huku yeye pia akilalamikiwa kwa kutokuelewana na wachezaji wake wakiongozwa na Paul Pogba.

Hata hivyo Mourinho ameongeza kuwa hafikirii kustaafu kufundisha kabumbu kwani umri wake bado mdogo na siku si nyingi atarejea kufundisha kandanda kwenye timu kubwa.