Modric ashinda tuzo ya Ballon D’or

0
1971

Luka Modric ameshinda tuzo ya Mwanasoka bora duniani ya Ballon D’or na kuwa mchezaji wa kwanza kushinda tuzo hiyo mbele ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Croatia ameshinda mataji matatu mfululizo ya ligi ya mabingwa Barani Ulaya akiwa na klabu yake ya Real Madrid na kisha kuisaidia nchi yake kufika fainali ya kome la FIFA la dunia mwezi Julai mwaka huu huko Russia.

Mshambuliaji wa Juventus, – Cristiano Ronaldo ameshika nafasi ya pili huku nyota wa FC Barcelona, – Lionel Messi akishika nafasi ya tano nyuma ya nyota wa Atletico Madrid , – Antoine Griezmann na mshambuliaji kinda wa PSG, – Kylian Mbappe ambao kwa pamoja waliisaidia Ufaransa kunyakua ubingwa wa dunia.

Luka Modric amesema tuzo hiyo ni kwa ajili ya wachezaji wote waliostahili kushinda, lakini waliikosa katika kipindi cha miaka kumi iliyotawaliwa na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo ambapo mchezaji wa mwisho kushinda tuzo hiyo kabla ya utawala wa wawili hao alikuwa mshambuliaji wa AC Milan, – Ricardo Kaka mwaka 2007.

Modric ameongeza kuwa inawezekana katika kipindi cha miaka kumi iliyopita kuna baadhi ya wachezaji walistahili kushinda tuzo ya Ballon D’or akiwemo Xavi Hernandes, Andres Iniesta na Wesley Sneijder, lakini watu sasa wanamshuhudia mtu mwingine.

Kiungo huyo wa Real Madrid amesema kuwa ni vigumu kuelezea hisia alizonazo baada ya kushinda tuzo hiyo kwani ni kitu cha kipekee kwake huku akiwataja Ronaldo na Messi kama wachezaji wa kipekee na kwamba kushinda tuzo hiyo mbele yao kunaonesha alifanya jambo la maana uwanjani kwa mwaka huu.

Naye mshambuliaji wa Olympic Lyon na timu ya Taifa ya Norway, – Ada Hegerberg amekuwa mwanamke wa kwanza kushinda tuzo ya Ballon D’OR ambayo kwa mara ya kwanza imetolewa kwa wanawake huku Kylian Mbappe akiwa mchezaji wa kwanza kinda kushinda tuzo hiyo kwa wachezaji wenye umri wa chini ya miaka 21, tuzo inayopigiwa kura na nyota waliowahi kushinda tuzo ya Ballon D’OR miaka iliyopita.