Kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana wa umri wa chini ya miaka 17 (Serengeti Boys), – Oscar Mirambo amelia na umri mkubwa wa wachezaji wa kikosi cha timu ya Taifa ya vijana ya Guinea kwenye mchezo wa kwanza wa mashindano ya Uefa Assist yanayofanyika nchini Uturuki.
Mirambo amesema kuwa kwa kiasi fulani maumbo ya wachezaji wa Guinea na namna wanavyocheza mpira wanaonekana wana umri mkubwa na umewafaidisha kupata matokeo mazuri dhidi ya vijana wake.
Serengeti Boys imepoteza mchezo huo kwa kufungwa bao moja kwa bila kupitia kwa Conte Aboubacaraliyefungakwenye kipindi cha kwanza ambacho kwa kiasi kikubwa kilitawaliwa na Guinea huku Serengeti Boys ikirejea mchezoni kwenye kipindi cha pili.
Licha ya kurejea mchezoni, lakini jitihada za Serengeti Boys hazikuzaa matunda kwani hawakufanikiwa kupata bao kwenye mchezo huo uliopigwa kwenye uwanja wa Emri Complex mjini Antalya, -Uturuki.
Serengeti Boys itashuka tena dimbani Jumatano Machi Sita mwaka huu kuwavaa Australia katika mchezo wa pili wa kundi A, ambapo mchezo huo utachezwa majira ya saa tisa alasiri.
Mchezo wa mwisho kwa Serengeti Boys katika hatua ya makundi na wa mwisho kwao kwenye mashindano hayo utakuwa dhidi ya wenyeji Uturuki utakaochezwa Ijumaa Machi Nane mwaka huu.
Guinea ni miongoni mwa timu shiriki za fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri wa chini ya miaka 17 zitakazofanyika nchini Tanzania mwezi Aprili mwaka huu ambapo imepangwa kundi B na timu za Cameroon, Morocco na Senegal huku mwenyeji Tanzania ikiwa kwenye kundi A na timu za Nigeria, Angola na Uganda.