Michuano ya Challenge kutofanyika mwaka huu

0
1590

Baraza la Vyama Vya Soka kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limethibitisha kutofanyika kwa michuano ya kombe la Challenge kwa mataifa wanachama kwa mwaka 2018 kutokana na sababu zilizo nje ya baraza hilo.

Katibu Mkuu wa CECAFA, – Nicholas Musonye amesema kuwa wamefanya kila linalowezekana kupata nchi muandaaji baada ya Kenya kujitoa bila mafanikio.

Kenya walipewa uenyeji wa michuano hiyo kwa mara ya pili baada ya mwaka 2017 kuifunga Zanzibar kwa changamoto ya mikwaju ya penati kwenye mchezo wa fainali na kunyakua taji hilo.

Musonye ameongeza kuwa wamejaribu kutafuta nchi mbadala ya kuandaa bila mafanikio, lakini muda pia umekuwa finyu kutokana na ratiba ya mashindano ya vilabu Barani Afrika ambapo sasa itaanza mwezi Novemba hadi Disemba mwaka huu kwenye hatua za awali.

Katika hatua nyingine, Musonye amethibitisha kufanyika kwa mashindano ya CECAFA kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka ishirini kuanzia Disemba 15 hadi 23 nchini Uganda.