Messi na mkasa wa kadi nyekundu

0
367

Lionel Messi ameoneshwa kadi nyekundu ya kwanza katika maisha yake ya kusakata kabumbu ndani ya FC Barcelona katika mchezo wa fainali ya Super Cup, mchezo ambao Barca wamepoteza kwa kunyukwa mabao matatu kwa mawili na Athletic Bilbao.

Super Cup ni taji ambalo lilianzishwa mwaka 1982 nchini Hispania ambapo timu Nne, yani mbili zilizomaliza katika nafasi za juu kwenye ligi na mbili zilizofika fainali ya kombe la mfalme maarufu kama Copa De La Rey huchuana kuwania taji hilo.

Messi ambaye alikuwa akicheza mchezo wa 753 akiwa na jezi ya FC Barcelona ameoneshwa kadi hiyo nyekundu katika kipindi cha pili cha dakika 30 za nyongeza baada ya kumpiga ngumi mchezaji wa Athletic Bilbao,  tukio lililopitiwa kwa umakini na teknolojia ya maamuzi kwa msaada wa video VAR.

Nyota huyo mwenye umri wa  miaka 33, amewahi kuoneshwa kadi nyekundu mara mbili katika maisha yake ya soka na zote alioneshwa akiwa na timu yake ya taifa ya Argentina.

Ya kwanza Messi alioneshwa mwaka 2015 dhidi ya Hungary huku ya pili akioneshwa mwaka 2019 katika mchezo wa kuwania nafasi ya tatu ya michuano ya Copa America dhidi ya Chile.

Baada ya kadi nyekundu ya jana, sasa Messi atakosa michezo minne ya ligi daraja la kwanza nchini Hispania maarufu kama La Liga kutokana na kanuni zinaoelekeza kuwa adhabu inayotolewa kwenye michuano hiyo itaendelea kutumika na kwenye ligi.

Kipigo cha usiku wa jana kinawafanya Barcelona kupoteza nafasi ya kushinda taji la 14 la Super Cup ambalo lingekuwa taji la kwanza kwa kocha Ronald Koeman lakini pia lingekuwa taji la nane la Super Cup kwa Messi kushinda akiwa na Barcelona,  taji ambalo pengine lingekuwa la mwisho kwake akiwa na miamba hiyo la Catalunya kutokana na tetesi kuwa huenda Messi akatimka Camp Nou mwishoni mwa msimu huu mkataba wake utakapomalizika.

Kwa upande wao Athletic Bilbao hili linakuwa taji lao la pili kushinda tangu mwaka 1985, lakini pia wanapata ushindi mfululizo dhidi ya Real Madrid na FC Barcelona kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1960.