Mane,Salah waafrika pekee kikosi cha FIFA

0
1235

Sadio Mane wa Senegal na Mohammed Salah wa Misri ni wachezaji wawili pekee kutoka barani Afrika waliotajwa kwenye orodha ya wachezaji 55 wanaowania nafasi ya nyota 11 watakaounda kikosi bora cha shirikisho la soka duniani FIFA.

Nyota hao wanaocheza soka la kulipwa kwenye klabu ya Liverpool msimu uliopita walicheza fainali ya ligi ya mabingwa barani ulaya dhidi ya Real Madrid lakini pia waliyawakilisha mataifa yao kwenye fainali za kombe la FIFA la dunia huko Russia ingawa mataifa yao hayakufanya vizuri.

Katika orodha hiyo mabingwa wa dunia Ufaransa wameingiza wachezaji Saba ambao ni Antoine Griezmann, N’golo Kante , Kylian Mbappe, Benjamin Pavard, Paul Pogba, Samuel Umtiti na Raphael Varane huku England ikiwa na wachezaji watatu akiwemo mfungaji bora wa kombe la FIFA la dunia Harry Kane.

Mshambuliaji wa mabingwa wa ulaya Real Madrid, Gareth Bale, hayupo kwenye orodha hiyo licha ya kufunga mabao mawili kwenye mchezo wa fainali ya ligi ya mabingwa barani ulaya dhidi ya Liverpool huku Cristiano Ronaldo aliyetimkia Juventus na mlinda mlango Thibaut Courtois aliyejiunga na Madrid akitokea Chelsea wakiingia kwenye orodha hiyo.

Orodha hiyo imepatikana baada ya majumuisho ya kura zilizopigwa na wachezaji 25,000 kutoka mataifa 65 duniani na orodha ya mwisho itakayotoa wachezaji 11 watakaounda kikosi cha bora cha FIFA itatangazwa September 24 jijini London wakati wa hafla ya utoaji tuzo ya mwanasoka bora wa dunia wa FIFA.