Mama mzazi wa Feisal Salum (Fei Toto) amesema kuwa mwanaye hana furaha wala hamu ya kurejea Yanga SC na wao kama familia wapo pamoja naye.
Katika mahojiano na televisheni moja ya mtandaoni mzazi huyo amesema, wanachotaka wao ni kuona Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litatoa uamuzi wa haki katika shitaka kati ya Yanga SC na Fei Toto.
“Fei kadhalilika sana … na alikuwa anajituma kwa sababu ya ndugu zake … kwa sababu alikuwa anajua nikisha kukaa kitako [kustaafu] hawa watanisaidia,” ameeleza.
Ameongeza kuwa Fei amedai haki yake kwa sababu siku za mbeleni endapo angeumia asingekuwa na thamani tena “hivyo kama familia kwanza sisi tupo pamoja na Fei kwa kumwombea kwa Mungu amsimamie, hili jambo liishe kwa salama na haki yake aipate.”
TFF inatarajia kutoa uamuzi leo kuhusu hatma ya nyota huyo kuvunja mkataba na klabu hiyo katika utaratibu ambao umeelezwa kuwa haukuhusisha pande mbili.