Makundi kombe la klabu bingwa Afrika kujulikana Disemba 28

0
884

Droo ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Afrika inatarajiwa kufanyika Ijumaa Disemba 28 makao makuu ya shirikisho la soka barani Afrika-Caf jijini Cairo nchini Misri.

Katika droo hiyo wawakilishi wa Tanzania katika michuano hiyo ambao pia ni wawakilishi pekee kwa nchi za Afrika Mashariki, timu ya Simba itawakilishwa na mwenyekiti wa bodi ya klabu hiyo Swed Nkwabi.

Shirikisho hilo limepanga poti ama vyungu vinne ambapo kila chungu kina timu 4 huku kila poti itatoa timu moja kuunda kundi moja.

Poti hizo zimepangwa kulingana na matokeo chanya ya klabu kwa miaka mitano iliyopita katika ligi ya mabingwa barani Afrika na michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika.

Chungu cha kwanza kina timu za Tp Mazembe Englebert kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yenye alama 66, Al Ahly ya Misri yenye alama 62, Wydad Casablanca ya morocco yenye alama 51 na Esperance Sportive De Tunis ya Tunisia yenye alama 45.

Chungu cha pili kina timu za Mamelodi Sundowns ya Afrika kusini yenye alama 40, As Vita club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yenye alama 29, Horoya ya Guinea yenye alama 19 na club African ya Tunisia yenye alama 12.

Katika chungu cha tatu kina timu za Asec Mimosas ya Ivory Coast yenye alama 8.5, Orlando Pirates ya Afrika Kusini yenye alama 8, fc Constantine ya algeria na fc platinum ya Zimbabwe zenye alama sifuri.

Na katika chungu cha nne kuna timu za Simba ya Tanzania, Lobi Stars ya Nigeria , Ismaily ya Misri na Js Saoura ya Algeria zote zikiwa na alama sifuri.

Kila chungu kitatoa timu moja kwa kila kundi huku timu zilizo katika poti moja haziwezi kupangwa kundi moja na kutakuwa na makundi manne yenye timu nne na kila timu itacheza mechi 6 ikiwa mechi 3 za nyumbani na mechi 3 za ugenini.

Mechi za makundi zitaanza Mwezi Januari hadi Machi ambapo mechi za kwanza kwenye kundi zitachezwa kati ya Januari 11 hadi 13, mechi za pili kwenye kundi zitachezwa kati ya Januari 18 hadi 20 ,mechi za tatu zikipangiwa kuchezwa kati ya Februari MOSI hadi TATU wakati mechi za nne zitachezwa kati ya Februari 12 hadi 13, mechi za tano kwenye kundi zitachezwa kati ya machi 8 hadi 11 na mechi za mwisho kwenye kundi zitachezwa kati ya machi 15 hadi18.

Timu mbili zitakazomaliza kwenye nafasi ya juu kwenye kila kundi zitafuzu kucheza robo fainali ya michuano hii ya ligi ya mabingwa barani Afrika na droo ya Robo fainali na nusu fainali itafanyika Cairo Misri March 23.

Mechi za Robo fainali zitachezwa kati ya April 5 hadi 7, nusu fainali kati ya Aprili 26 hadi 28 na fainali itachezwa kati ya Mei 24 na 25.