Lopetegui atimuliwa Madrid

0
2003

Klabu ya Real Madrid imemtimua kocha wake Julen Lopetegui ikiwa imepita miezi minne na nusu tangu alipopewa kibarua cha kukinoa kikosi hicho.

Mhispania huyo alirithi mikoba iliyoachwa na Zinedine Zidane mwezi June mwaka huu, lakini kipigo kizito cha mabao matano kwa moja kutoka kwa mahasimu zao FC Barcelona kwenye mchezo wa El Clasico kimeondoa uvumilivu wa mabosi wa miamba hiyo na kuamua kumtimua.

Uamuzi wa kumfungashia virago Lopetegui umekuja saa chache baada ya kikao cha bodi ya wakurugenzi wa timu hiyo chini ya Rais wa Real Madrid, –  Florentino Perez ambaye baada ya mchezo wa El Clasico alitoka uwanjani akiwa amekasirika.

Hii ni mara ya pili kwa kocha Lopetegui kufukuzwa kazi ndani ya kipindi cha mwaka mmoja baada ya kuondoshwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Hispania  kwenye kombe la Dunia huko Russia  siku mbili baada ya kugundulika kuwa yupo katika mazungumzo ya mwisho ya kupata kibarua cha kuinoa Real Madrid baada ya mashindano ya kombe la dunia kumalizika.

Nyota wa zamani wa Real Madrid ambaye anakinoa kikosi cha pili cha timu hiyo Santiago Solari ameteuliwa kuwa kocha wa muda wa Madrid baada ya mazungumzo na aliyekuwa kocha wa Chelsea, -Antonio Conte kuchelewa na kibarua chake cha kwanza kitakuwa Jumatano wiki hii atakapoiongoza Madrid kwenye mchezo wa kombe la mfalme dhidi ya Melilla.