Liverpool wamepata ushindi wa Tatu dhidi ya Chelsea katika michezo 17 waliyokutana katika miaka ya hivi katribuni, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao Mawili kwa Bila kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya England uliochezwa kwenye dimba la Anfield.
Mshambuliaji wa Kimataifa wa Senegal, Sadio Mane alianza kuiandikia Liverpool bao la kuongoza katika dakika ya 51 kabla ya Mohamed Salah kupigilia msumari wa mwisho kwa bao safi katika dakika ya 53 na kuirejesha Liverpool kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Kipigo hicho kinawafanya Chelsea kupoteza michezo Sita ya ugenini dhidi ya timu Sita za juu kwenye ligi ya England huku wakiruhusu kufungwa mabao 16, lakini huku majogoo wa jiji Liverpool ukiwa ni ushindi wao wa kwanza dhidi ya The Blues kwenye dimba la Anfield tangu waliposhinda kwa mabao Manne kwa Moja mwezi Mei mwaka 2012.
Ushindi wa Liverpool unazidi kukoleza mbio za kuufukuza ubingwa kati yao na matajiri Manchester City ambapo tofauti ya alama kati yao ni Mbili, Liverpool wakiongoza wakiwa na alama 85 huku City wakiwa katika nafasi ya pili na alama 83 ingawa Liverpool wamecheza mchezo mmoja zaidi ya Manchester City.
Ligi hiyo inaendelea tena hii leo Jumatatu kwa mchezo mmoja kuchezwa ambapo washika bunduki wa jiji la London, -Arsenal wanaowania nafasi ya kumaliza miongoni mwa timu Nne za juu, watakuwa ugenini kumenyana na timu ngumu ya Watford katika mchezo utakaochezwa kwenye dimba la Vicarage.