Ligi ya soka ya wanawake yaendelea nchini

0
452

Kivumbi cha ligi kuu ya wanawake Tanzania bara kinaendelea leo kwa michezo sita ya mzunguko wa pili kuunguruma kwenye viwanja tofauti kuanzia majira ya saa kumi jioni.

Kwenye dimba la Isamuhyo jijini Dar Es Salaam bingwa mtetezi JKT Queens wanashuka dimbani kuwaalika Tanzanite ya Arusha wakati Evergreen Queens wakiwa wenyeji wa Simba Queens mchezo utakaochezwa kwenye dimba la Karume jijini Dar Es Salaam huku Yanga Princes wakisafiri hadi kwenye dimba la Nyamagana jijini Mwanza kumenyana na Marsh Queens.

Michezo mingine itawakutanisha Sisters ya Kigoma wakiwa kwenye dimba la Lake Tanganyika kuwakaribisha Baobab ya Dodoma wakati kwenye dimba la Mabatini pale Mlandizi – Kibaha mkoani Pwani wenyeji Mlandizi Queens watachuana na Alliance Girls huku Panama wakiwa nyumbani kwenye dimba la Samora mjini Iringa kumenyana na Mapinduzi Queens.

Mpaka sasa bingwa mtetezi wa ligi hiyo JKT Queens wanaongoza kwenye msimamo wakiwa na alama 3 na faida ya magoli 9 ya kufunga waliyopata kwenye mchezo wa kwanza wakifuatiwa na Alliance Girls, Mlandizi Queens, Marsh Queens, Simba Queens na Sisters ya Kigoma wenye alama tatu kila mmoja huku Evergreen ya Dar Es Salaam ikiburuza mkia.