Ligi ya mabingwa Barani Ulaya kutimua vumbi

0
2045

Msimu mpya wa ligi ya mabingwa barani Ulaya unaanza kutimua vumbi usiku wa Septemba 18 kwa kupigwa michezo nane ya makundi Aaa mpaka Dee.

Katika michezo inayotazamiwa kuwa na mvuto mkubwa ni pamoja na ule utakaowakutanisha majogoo wa jiji Liverpool na Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa katika mchezo wa kundi Che.

PSG ina matumaini ya nyota wake NEYMAR kuanza kwenye mchezo huo baada ya kupumzishwa kwenye mchezo uliopita wa ligi daraja la kwanza pale nchini Ufaransa.

Liverpool wao wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa hawana uhakika wa asilimia mia kama nyota wao, Mbrazil Roberto Firmino anayeugulia maumivu ya jicho baada ya kuchokolewa na mlinzi wa Tottenham – Jan Vertonghen kwenye mchezo ligi kuu ya England wikiendi iliyopita.

Liverpool inaanza kampeni ya ligi ya mabingwa Barani Ulaya ikiwa na kumbukumbu ya kushindwa kutwaa taji hilo ilipofika fainali ya michuano hiyo msimu uliopita baada ya kunyukwa na REAL Madrid mabao matatu kwa moja.

Katika mchezo mwingine wa kundi Che, Napoli ya Italia itakuwa ugenini kumenyana na Redstar Belgrade ya Serbia.

Michezo mingine ni pamoja na ile ya kundi Aaa ambapo Club Brugge ya Ubelgiji inaialika Borussia Dortmund ya Ujerumani huku Monaco ya Ufaransa itakuwa mwenyeji wa bingwa wa Uefa Europa League msimu uliopita, Atletico de Madrid ya Hispania.

Kwenye kundi Be, Barcelona ya Hispania itakuwa nyumbani kwenye dimba la Camp Nou kukipiga na Psv Eindhoven ya Uholanzi na Tottenham Hotspurs itakuwa ugenini kwenye dimba la Giuseppe Meazza kupepetana na Football Club Internazionale Milano maarufu kama Inter Milan.

Na kwenye kundi De, Galatasaray ya Ugiriki inamenyana na Lokomotiv Moscow huku Schalke 04 ya Ujerumani ikikipiga na FC Porto ya Ureno.

Ligi hiyo itaendelea tena kwa kupigwa michezo mingine nane ya makundi Eee hadi H ambapo kwenye kundi Eee Ajax ya Uholanzi itakuwa mwenyeji wa AEK Athens ya Ugiriki huku Benfica ya Ureno ikifungua dimba kwa kuwaalika Bayern Munich ya Ujerumani.

Machester City ya England itapepetana na Lyon ya Ufaransa katika mchezo wa kundi F huku Shakhtar Donetsk kutoka nchini Ukraine wakimenyana na TSG Hoffenheim ya Ujerumani katika mchezo mwingine wa kundi F.

Nako kwenye kundi G, bingwa mtetezi wa ligi hiyo, Real Madrid itaanza kampeni ya kulitetea tena taji lake kwa kumenyana na AS Roma ya Italia kwenye dimba la Santiago Bernabeu huku Viktoria Plzen ya Jamhuri ya Czech ikikipiga na CSKA Moscow ya Russia.

Na kwenye kundi H, Juventus ya Cristiano Ronaldo itakuwa ugenini nchini Hispania kukipiga na Valencia huku Mashetani Wekundu, Manchester United ya England ikisafiri hadi nchini Switzerland kumenyana na Young Boys.