Ligi Kuu Tanzania Bara yaingia raundi ya Tano

0
2034

Ligi Kuu Tanzania Bara inaingia kwenye raundi yake ya Tano huku timu zingine zikicheza michezo yake ya raundi ya tatu kwenye msimu wa 2018/2019.

Kwenye dimba la Taifa jijini Dar es salaam, mabingwa wa kihistoria Yanga watakuwa wenyeji wa wagosi wa kaya Coastal Union ya Tanga ambayo imerejea msimu huu kwenye ligi kuu baada ya kuikosa kwa misimu miwili.

Yanga ambao mchezo huo dhidi ya Coastal Union utakuwa wa tatu kwao, wameshashinda michezo miwili iliyocheza, huku Coastal Union ikicheza michezo minne na imeshinda mchezo mmoja na kutoka sare michezo mitatu.

Huko Musoma – Mara kwenye dimba la kumbukumbu ya Karume, timu ngeni kwenye ligi kuu Biashara United yenyewe itawaalika matajiri wa Chamazi Azam FC huku wanakuchele Ndanda FC baada ya kutoka sare na mabingwa watetezi Simba safari hii wana kibarua kingine kigumu mbele ya mabingwa wa kombe la Shirikisho, -Mtibwa Sugar.

Kwenye dimba la Samora mjini Iringa, wanapaluhengo Lipuli FC ambayo haijashinda mchezo hata mmoja ikiwa imetoka sare kwenye michezo yake yote minne iliyocheza safari hii, inakipiga na timu inayoburuza mkia kwenye ligi kuu Alliance FC ya Mwanza.

Jijini Mbeya, Wagonga nyundo au watoza ushuru wa jiji hilo Mbeya City watawaalika wazee wa kupapasa Ruvu Shooting na mchezo wa mwisho kwa Septemba 19 utapigwa kwenye migodi ya Almasi huko Mwadui mkoani Shinyanga ambapo wenyeji Mwadui FC watawaalika vinara wa ligi kuu kwa sasa JKT Tanzania.