Kubadili mdhamini Simba, chanzo cha jezi kuchelewa

0
322

Kampuni ya Vunjabei imesema kuwa sababu kubwa ya kuchelewa kwa jezi za Simba SC msimu huu ni kubadilishwa kwa mdhamini wa klabu ambako kulipelekea muda mwingi kutumika katika kuandaa mkataba.

Akizungumza na kituo cha redio cha EFM, Fred Fabian Ngajiroalso ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Vunjabei Group of Companies amesema kuwa licha ya kuchelewa huko, lakini manufaa waliyoyapata ni kwamba wamepata mkataba mzuri wa TZS bilioni 26 kwa miaka mitano, jambo ambalo ni bora kuliko wangeharakisha mkataba ili wawahishe jezi.

“Ule mkataba ulichukua muda mrefu sana, mpaka wamekuja ku-comfirm [idhinisha] jezi ni mwezi wa sita mwishoni […] ingekuwa hatukubadilisha mdhamini jezi zingekuwa zimefika mapema, kila mtu angekuwa amepata jezi, na hakungekuwa na shida yoyote.” amesema Vunjabei

Aidha, amesema sababu nyingine zilizochangia ni changamoto za usafiri zilizochangiwa na uchaguzi mkuu wa Kenya, sensa ya watu na makazi na kombe la dunia ambapo alipata changamoto ya kusafirisha mizigo ya jezi kwani meli na ndege zilikuwa zikibeba mizigo kwa kazi hizo tatu.

Amewatoa hofu mashabiki wa Simba kwamba kuanzia Agosti 15 mwaka huu mashabiki wote wa timu hiyo mkoani Dar es Salaam watakuwa wamepata jezi kwani zinaendelea kuletwa.