Beki wa kimataifa wa Ufaransa na klabu ya Arsenal, – Laurent Koscielny ametangaza kustaafu rasmi soka la kimataifa huku akimkosoa vikali kocha wa timu ya Taifa ya nchi hiyo Didier Deschamps kuwa hakumjali katika kipindi alichokuwa akiuguza jeraha lake.
Koscielny alipata majeraha ya nyama za paja wakati wa mchezo wa nusu fainali ya michuano ya Yuropa mwezi Mei mwaka huu na kukosa fainali za kombe la FIFA la dunia zilizofanyika nchini Russia na taifa lake kutwaa ubingwa.
Katika taarifa yake, Koscielny amesema kuwa watu wengi wamemfedhehesha wakati akiuguza majeraha yake kitendo ambacho amekifananisha na maumivu makali kwenye kisogo.
Beki huyo ameongeza kuwa wakati ukiwa kwenye kiwango bora unapata marafiki wengi sana lakini ukiwa majeruhi baada ya muda unasahaulika kabisa, na kutolea mfano kocha wake Deschamps kuwa katika kipindi chote amempigia simu mara moja tu wakati wa sikukuu yake ya kuzaliwa na baada ya hapo hakuwahi hata kupata salamu yake.
Koscielny ameichezea Ufaransa katika michezo 51 tangu mwezi Novemba mwaka 2011 na alikuwa kwenye kikosi cha Ufaransa kwenye michuano ya Ulaya ya mwaka 2012 na 2016 pamoja na Kombe la Dunia la mwaka 2014 nchini Brazil.