Kocha wa Serengeti Boys avitwisha jukumu vilabu vya Tanzania

0
271

Kocha wa timu ya taifa ya mpira wa miguu kwa vijana chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) amevitaka vilabu mbalimbali nchini Tanzania kuwachukua na kulea vipaji vya vijana hao, ili taifa liweze kuwa na vijana wenye vipaji na mafunzo wakati wote.

Habibu Omari ametoa rai hiyo wakati akizungumzia maandalizi ya timu yake kuelekea michuano ya Mataifa ya Afrika chini ya miaka 17 itakayofanyika nchini Morocco kuanzia Julai 2021.

Amesema kuwa vijana wenye vipaji wapo, lakini huko mikoani hawapo kwenye timu yoyote wanayopewa mafunzo, hivyo ni vyema timu zenye dhamana zikawachukua na kukuza vipaji vyao.

Hata hivyo amesema mpango wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni kuwa na timu za miaka 17, 18, 19 na 20, ili kuhakikisha vipaji vya vijana hao havifi na pia kuweza kuinua soka la Tanzania.

Kuhusu uchaguzi wa wachezaji wa timu hiyo amesema kuwa wamezunguka mikoa mbalimbali na kwamba wanaamini timu hiyo inawakilisha sura ya taifa kwa kuwa na wachezaji kutoka maeneo mbalimbali.

Amesema anaamini kuwa U17 itafanya vizuri kwenye mashindano ya mwaka huu kuliko ilivyofanya mwaka 2018 ambayo Tanzania ilikuwa mwenyeji.