Timu ya KMC ya Tanzania na ile ya AS Kigali ya nchini Rwanda, zimetambiana kufanya vizuri katika mchezo wa Kimataifa wa Kombe la Shirikisho utakaopigwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Kocha Msaidizi wa timu ya KMC, – Mrage Kabange amesema kuwa kutokana na mazoezi waliyofanya, anaamini wataibuka na ushindi huku kocha wa timu ya AS Kigali, -Shimnyama Erick naye akisema kuwa ushindi kwao ni wa lazima.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa nchini Rwanda, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana.
Ili isonge mbele katika hatua inayofuata, timu ya KMC ni lazima ishinde mchezo huo.
Wakati timu ya KMC ikicheza siku ya Ijumaa, nayo timu ya Azam ambayo ni Wawakilishi wa Tanzania katika Michuano ya Kombe la Shirikisho, itashuka dimbani siku Jumamosi katika uwanja wa Azam Complex, kucheza na timu ya Fasil Kenema ya Ethiopia na Yanga itakuwa ugenini siku hiyo hiyo kucheza na Township Rollers ya Botswana.
Wekundu wa Msimbazi Simba, wao watakuwa nyumbani siku ya Jumapili kuwakaribisha UD Songo ya Msumbiji katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.