Wachezaji wa timu ya KMC FC tayari wamewasili kambini kwa ajili ya maandalizi ya kuelekea katika msimu mpya wa 2022/2023 utakaoanza Agosti 17 mwaka huu kwa mujibu wa ratiba ya Bodi yad Ligi Kuu Tanzania (TPLB).
Wachezaji waliowasili kambini hadi sasa ni maingizo mapya waliosajiliwa msimu huu, na wale ambao walikuwa kwenye mipango ya kocha Mkuu Thierry Hitimana mara baada ya kumalizika kwa msimu wa 2021/2022.
Kwa sasa KMC itaweka kambi mkoani Dar es Salaam kujiandaa na msimu mpya huku ikiendelea kujifua zaidi kutokana na programu ambazo kocha mkuu Hitimana ameandaa kwa ajili ya kuwajenga wachezaji kabla ya kuanza kwa msimu mpya Agosti 17.
Katika kipindi hiki cha maandalizi ya msimu mpya kwa mujibu wa programu ya kocha Hitimana, kutakuwa na mechi nyingi za kirafiki, mazozi ya uwanjani kwa awamu mbili ambazo ni uwanjani pamoja na Gym.
Timu hiyo ya manispaa ya Kinondoni hadi sasa imeachana na wachezaji 10 ambao ni Hassan Kessy, Hassan Kabunda, Ally Ramadhani Oviedo, Sudi Dondola, Denis Richard, Jeani Mugiraneza,Hassan Kapalata, Nickson Kibabage, Martin Kigi pamoja na Abasi Kapombe.