Kenya inatarajia kuungana na Tanzania na Uganda katika mchakato wa kuomba kuwa mwenyeji wa shindano la Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.
Akizungumza leo Ikulu jijini Nairobi, Rais wa Kenya, William Ruto amesema Taifa hilo lina vipaji vingi vinavyohitaji kukuzwa.
“Tumeungana na ndugu zetu wa Tanzania na Uganda katika kutuma ombi la pamoja kwenda Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa ajili ya fursa ya kuwa mwenyeji wa AFCON 2027. Kati ya nchi hizi hakuna iliyowahi kupata fursa ya kuwa mwenyeji wa mashindano haya makubwa Afrika,” amesema Ruto.
Katika mashindano hayo, Uganda imefuzu mara saba, Kenya imefuzu mara tano huku Tanzania ikifuzu mara mbili.