Kambi ya Stars yaongeza nguvu

0
621

Wachezaji watu wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, wameshajiunga na kambi ya timu ya taifa ya soka ya Tanzania – Taifa Stars iliyoko nchini Afrika Kusini.

Wachezaji walioripoti kambini ni walinzi Abdi Banda anayecheza soka kwenye timu ya Baroka FC ya nchini Afrika Kusini, Hassan Kessy anayecheza soka nchini Zambia kwenye timu ya Nkana Ranger pamoja na mshambuliaji Rashid Mandawa anayecheza soka nchini Botswana.

Wachezaji wengine wanaocheza soka nje ya nchi wanaotarajiwa kujiunga na kambi hiyo ni nahodha Mbwana Samatta wa Genk ya Ubelgiji, nahodha msaidizi Himid Mao wa Petrojet ya Misri, Simon Msuva anayecheza soka nchini Morocco kwenye timu ya Hassan Difa El Jajida na mshambuliaji Shaaban Idd Chilunda anayecheza soka nchini Hispania kwenye timu ya Tenlif.

Hii ni wiki ya pili tangu Stars iweke kambi nchini Afrika kusini kwenye mji wa Bloemfontein uliopo kwenye jimbo la Free State kwa lengo la kujiandaa na mchezo muhimu wa kufuzu kwa michuano ya Afrika (AFCON) dhidi ya Lesotho.

Mchezo huo utachezwa jumapili ijayo kwenye mji mkuu wa Lesotho, – Maseru ambapo Taifa Stars inatakiwa kushinda mchezo huo ili kufuzu kwa mara ya pili kwenye michuano hiyo ya mataifa ya Afrika.