Je, Prince Dube anakwenda Simba au Yanga?

0
782

Baada ya mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube kuandika barua akitaka kuvunja mkataba na matajiri hao wa Dar es Salaam, tetesi za wapi atakapokwenda zimekuwa nyingi.

Baadhi ya mashabiki na wanazi wa soka kupitia mitandao ya kijamii wameandika kuwa huenda mwanamfalme huyo, raia wa Zimbabwe akaibukia katika moja ya miamba ya soka ya Kariakoo.

“Prince DUBE to YANGA SC ni suala la Muda tu, WANANCHI wapo tayari kuvunja Mkataba wa Milioni 765,” ameandika Marco Mzimbe kupitia X huku Charlie Bihemo yeye akisema “Karibu Simba Prince Dube. Yule Ostaz Freddy Michael aondoke.”

Ukurasa wa SportArenaTz kupitia mtandao wa X umeandika; “YANGA wanahitaji sana huduma ya mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube. Wanaamini Dube anaweza kuwa mtu sahihi wa kuziba nafasi ya Fiston Mayele […] Habari za ndani ni kwamba kuna mfanyakazi mmoja wa Yanga ambaye hapo kabla alikuwa Azam ndiye anayechora ramani ya Dube kuhamia Yanga.”

Wakati hayo yakiendelea, mjadala mwingine ulioibuka ni kuhusu utaratibu wa uvunjaji mkataba, baadhi wakifananisha tukio hilo na kilichotokea kwa Feisal Salum (Fei Toto) wakati akihama kutoka Yanga kwenda Azam.

Je, wewe una maoni gani kuhusu Dube kutaka kuondoka Azam? Unadhani anataka kwenda klabu gani?