Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inaratibu mpango wa kutoa mafunzo ya ukocha kwa wanafunzi wa vyuo vinavyotoa mafunzo ya michezo ikiwemo chuo cha maendeleo ya michezo Malya, Butimba na vyuo vikuu nchini.
Hayo yamesemwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul wakati akijibu swali la Antipas Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, aliyetaka kufahamu kwa nini makocha wa mpira wa miguu Tanzania hawafundishi nje ya nchi hata katika ukanda wa Afrika Mashariki au nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Naibu Waziri Gekul amesema, kwa sasa Tanzania ina makocha 19 wenye viwango vya CAF ‘A’ Diploma ambapo wanakidhi viwango vya kufundisha nje ya nchi.
“Makocha hawa hawafanikiwi kupata fursa ya kufundisha nje ya nchi kutokana na historia ya elimu walizonazo.” amesema Naibu Waziri Gekul
Hata hivyo Naibu Waziri Gekul amesema upo mkakati wa kuhakikisha kwenye michezo ya vipaumbele ya kitaifa wanapatikana pia makocha wanawake.