Ligi ya kulipwa ya mpira wa kikapu nchini Marekani ya NBA imeendelea ambapo bingwa mtetezi Golden State Warriors wameendeleza wimbi la ushindi kwa kuinyuka Los Angeles Clippers alama 129 kwa 127 kwenye mchezo uliochezwa kwenye dimba la Oracle mjini Oakland – California.
Nyota wa mchezo huo alikuwa Stephen Curry aliyefunga alama 42 huku Kevin Durant akifunga nyingine 35 na kucheza mipira iliyorudi uwanjani yaani rebounds 12 na kulizamisha jahazi la Clippers lililokuwa likiongozwa na Tobias Harris aliyefunga alama 32 na kucheza rebounds 9.
Wakati Warriors wakitakata makamu bingwa Cleveland Cavaliers wameendelea kupokea kipigo baada ya kunyukwa alama 112 kwa 92 na Chicago bulls.
Huu unakuwa mchezo wa 26 kwa Cavaliers kupoteza katika msimu huu, huku wakiwa wameshinda michezo 8 pekee na kuna wasiwasi kuwa huenda wakashindwa kufuzu kwa hatua ya mtoano yaani play off kama mambo yataendelea kuwaendea kombo.
Huko TD Garden mjini Boston – Massachusetts wenyeji Boston Celtics wameitandika Charlote Hornets alama 119 kwa 103 wakati Washington Wizards wakishindwa kutamba mbele ya Indiana Pecers na kula mweleka wa alama105 kwa 89 huku Orlando Magic wakikiona cha moto mbele ya Miami Heat kwa kutandikwa alama 115 kwa 91.