Fury alalamikia maamuzi mabovu

0
1594

Bondia Tyson Fury wa nchini Uingereza amesema kuwa dunia inatambua bingwa wa dunia wa uzito wa juu (WBC) ni nani, na anaamini sare aliyoipata Deontay Wilder wa Marekani dhidi yake ilikuwa ni maamuzi ya zawadi kwa Mmarekani huyo.

Fury mwenye umri wa miaka 30 alitoka sare kwenye pambano la kuwania ubingwa wa WBC kati yake na Wilder ingawa mabondia wengi wa Kimataifa wanasema kuwa Fury alishinda katika mpambano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Stapeles mjini Los Angeles, – Califoirnia.

Akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya pambano hilo,  Fury amesema kuwa hajawahi kushuhudia maamuzi mabovu ya mchezo wa masumbwi katika maisha yake kama maamuzi yaliyotelewa kwenye mpambano huo na kuongeza kuwa hajui majaji walikuwa wakiangalia pambano la aina gani.

Mabingwa wa zamani wa dunia akiwemo Floyd Mayweather, Lennox Lewis, Tony Bellew na Carl Froch wanaamini kuwa Fury alishinda pambano hilo ambalo baada ya raundi ya 12 majaji waliamua limalizike kwa sare.

Jaji wa kwanza alimpa Wilder ushindi wa alama115 kwa 111 huku jaji wa pili akimpa ushindi wa alama 114 kwa 112 na  jaji wa tatu akatoa alama 113 kwa kila mmoja.

Hata hivyo, muandaaji wa pambano hilo Frank Warren amesema kuwa yeye pamoja na bodi ya usimamiaji wa mchezo wa masumbwi nchini Uingereza wataandika barua kwa WCB kuomba mtanange huo urudiwe.