Dabi ya Simba na Yanga hatihati kutochezwa kwa Mkapa

0
439

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema kuwa kuna uwezekano mchezo wa Ligi Kuu ya NBC kati ya Simba na Yanga usichezwe katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kama ilivyozoeleka.

Saidi Yakubu amesema hayo katika kipindi cha Jambo Tanzania cha TBC1 akieleza kuwa uamuzi huo unatokana na mpango wa Serikali wa kufunga uwanja huo Machi 28 mwaka huu ili kutekeleza maboresho yaliyoainishwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Hata hivyo, amesema uamuzi wa kufunga uwanja haujafikiwa na kwamba inategemea na matokeo ya michezo ya kimataifa ya Simba na Yanga ambazo zote zinawania kufuzu hatua za robo fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, mtawalia.

“Timu zetu kama zikawa zimefikia mwisho, tutalazimika kuhamishia uwanja wa uhuru au sehemu nyingine ambapo bodi ya ligi itaamua,” ameeleza Yakubu.

Kuhusu maboresho ya ujumla ya uwanja amesema yametokana na mapendekezo ya CAF lakini haina maana kuwa uwanja una shida, akitolea mfano moja ya maboresho ni kuongeza idadi ya viti katika benchi la ufundi kutoka 12 vya sasa hadi 23, kufunga ‘screen’ ya kisasa itakayoonesha matokeo ya mchezo na idadi ya watazamaji yenyewe (automatic) pamoja na kuboresha eneo la kuchezea.