Corona yaathiri ligi ya Europa

0
1371

 
Michezo kadhaa ya ligi ya Europa imeahirishwa kutokana na tishio la virusi vya corona,  hasa nchini Italia.

Timu ya AS Roma ya Italia imekwama kusafiri kwenda nchini Hispania kucheza mchezo wa kombe la Europa dhidi ya  Sevilla, kwa sababu ya virusi hivyo ambapo ndege za Italia hazizihusiwi kutua nchini Hispania.

Mchezo huo wa mkondo wa kwanza wa michuano hiyo ya pili kwa ukubwa barani Ulaya kwa ngazi ya vilabu, ulitakiwa kuchezwa bila ya mashabiki kutokana na hofu ya virusi vya corona na sasa hautokuwepo kabisa.

Italia ni nchi ya kwanza kukumbwa na virusi vya corona nje ya China,  ambapo inadaiwa takribani watu elfu kumi wameambukizwa virusi hivyo.

Raia Milioni sitini wa Italia wametakiwa kubaki majumbani mwao ili kuzuia kuenea kwa virusi vya corona, huku michezo ya ligi ya Italia (SERIA A) pamoja na michezo mingine ikiwa imezuiwa kuchezwa nchini humo.

Mchezo mwingine uliofutwa ni kati ya Inter Milan ya Italia dhidi ya Getafe ya Hispania,  huku baadhi ya michezo ikitarajiwa kuchezwa usiku wa leo bila mashabiki.