City wapoteza kwa Lyon

0
1058

Kampeni ya Manchester City kwenye mashindano ya klabu bingwa barani Ulaya imeingia dosari baada kuanza vibaya kama mabingwa watetezi wa ligi kuu England kwa kupoteza mbele ya Lyon katika uwanja wa Etihad kwa kuchapwa mabao mawili kwa moja.

Maxwel Cornet aliifungia Lyon goli la kwanza baada ya makosa ya Fabian Delph ya kushindwa kuutoa mpira nje baada ya krosi iliyopigwa na Fekir.

City ambao wanapewa nafasi ya kufanya vizuri kwenye klabu bingwa walijikuta wakiongozwa kabla ya mapumziko.

Nahodha wa Lyon, -Fekir alifunga goli la pili umbali wa mita 25 baada ya makosa kutoka kwa Fernandinho.

Bernardo Silva aliwapa matumaini City baada ya kufunga goli akisaidiwa na Leroy Sane, lakini wenyeji walikosa bahati ya kupata mabao na hivyo kushindwa kuepuka kupoteza mchezo wao wa kwanza kwenye mashindano hayo makubwa Ulaya.

Pamoja na majaribio kadhaa kutoka kwa beki Aymerici Laporte, Gabriel Jesus na Sergio Aguero walishindwa kupata magoli kutokana na ubora wa mlinda mlango wa Lyon,- Anthony Lopes.

City ilionekana ikosa maelekezo muhimu kutoka kwa kocha mkuu Pep Guardiola kutokana na adhabu anayoitumikia.

Kocha wa Manchester city alikuwa anaushuhudia mchezo huo akiwa jukwaani akitumikia adhabu yake aliyoipata msimu uliopita katika hatua ya robo fainali dhidi ya Liverpool.

Kocha msaidizi Mikel Arteta ambaye pia ni kiungo wa zamani wa Arsenal alichukua majukumu ambayo hata hivyo yalionekana kumzidi.

City ilionekana kama wangeendelea kutawala soka la Ulaya baada ya kufanikiwa kupata alama mia moja katika msimu uliopita kwenye ligi kuu England, lakini hata hivyo watahitaji kupambana kwa hali na mali ili waweze kuongoza kundi lao kama walivyofanya msimu uliopita.