Cavaliers yaandamwa na matokeo mabovu

0
1622

Jinamizi la matokeo mabovu limeendelea kuwaandama makamu bingwa wa Ligi Kuu ya kulipwa ya mpira wa kikapu nchini Marekani (NBA) timu ya Cleveland Cavaliers baada ya kutandikwa alama 100 kwa 83 na Oklahoma City Thunder katika mchezo uliochezwa kwenye dimba la Chespeake Energy mjini Oklahoma City.

Nyota wa mchezo huo alikuwa Russel Westbroo aliyeifungia Oklahoma alama 23 na kucheza mipira iliyorudi yani Rebounds 19 huku akitoa pasi za kufunga 15 zilizotosha kulizamisha jahazi la Cavaliers lililokuwa likiongozwa na Jordan Clarkson aliyefunga alama 25.

Huo unakuwa mchezo wa 16 kwa Cavaliers kupoteza katika michezo 20 waliyocheza tangu kuanza kwa msimu huu, wakishika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Kanda ya Mashariki inayoongozwa na Toronto Raptors.

Cavaliers wameyumba kwa kiasi kikubwa baada ya kuondoka kwa aliyekuwa nyota wao Lebron James aliyetimkia Los Angeles Lakers.

Katika matokeo mengine , wakongwe Chicago Bulls wameshindwa kutamba ugenini baada ya kula mweleka wa alama 116 kwa 113 mbele ya Milwaukee Bucks wakati Washngton Wizards wakipokea kipigo cha alama 125 kwa 104 kutoka kwa New Orlean Pelicans huku Dallas Mavericks wakiinyuka Huston Rockets alama 128 kwa 108 na San Antonio Spurs wamelala kwa alama 128 kwa 89 mbele ya Minasota Timberwolves.

Huko Barclays Center mjini Brooklyn – New York, wenyeji Brooklyn Nets wamekiona cha moto kwa kutandikwa alama 101 kwa 91 na Utah Jazz wakati Philadelphia 76ERS wakiishikisha adabu New York Knicks kwa kuitandika alama 117 kwa 91 na Atlanta Hawks wameshindwa kutamba ugenini na kunyukwa alama 108 kwa 94 na Charlote Hornets.