Biashara United yabanwa mbavu na Kagera Sugar

0
236

Mchezo kati ya Biashara United dhidi ya wakata miwa wa Kagera (Kagera Sugar) umemalizika kwa kushuhudia sare ya mabao mengi katika uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara.

Kagera Sugar walikuwa wa kwanza kupata goli kupitia kwa Meshack Mwamita dakika ya kwanza ya mchezo, Dakika ya 32 baadae Erick Mwijage akaongeza bao la pili na kuwafanya Kagera kuwa na mtaji wa magoli mawili hadi mapumziko.

Dakika nne pekee za kipindi cha pili ziliwatosha Biashara United kuandika bao la kwanza kupitia kwa Collins Opare kwa mkwaju wa penati, Dakika ya 80 Baron Oketch akaweka mizani sawa baada ya kuongeza bao la pili na kufanya ubao usomeke 2-2.

Ambrose Awio akawatanguliza Biashara mguu mmoja kwenye pointi tatu baada ya kufunga bao la tatu dakika ya 82, lakini David Luhende akafanya wagawane pointi moja moja kwani dakika ya 90 akaisawazishia Kagera Sugar bao la tatu, na mpaka kipenga cha mwisho cha mwamuzi, Biashara United 3-3 Kagera Sugar.

Kwa matokeo hayo timu zote zimefikisha alama kumi na zinaendelea kusalia mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.