Arsenal na Chelsea zatinga 16 bora

0
827

Timu za Arsenal na Chelsea zimeungana na timu nyingine 14 kufuzu hatua ya 16 bora ya michuano ya ligi ya YUROPA baada ya kupata matokeo chanya katika michezo yao.

Arsenal wakicheza katika dimba lao la Emirates wamepindua matokeo na kuwanyuka Bate Borisov mabao matatu kwa bila na hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao matatu kwa moja.

Bao la kujifunga la Zakhar Volkov na mengine mawili ya Shkodran Mustafi na Sokratis  Papastathopoulos yametosha kuivusha Arsenal na kufuzu hatua hiyo ya 16 bora.

Katika matokeo mengine,  Genk ya Nahodha wa timu ya soka ya Tanzania (Taifa Stars), – Mbwana Samatta ikiwa katika dimba lake la nyumbani la Laminus Arena , imenyukwa mabao manne kwa moja na hivyo kuondoshwa kwa matokeo ya jumla ya mabao manne kwa moja.

Chelsea wamepata ushindi wa mabao matatu kwa bila dhidi ya Malmoe FF ya Sweden na kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao matano kwa moja.

Mabao ya Olivier Giroud, Ross Barkley na Cullum Hudson Odoi ndiyo yaliyoivusha Chelsea katika hatua hiyo ya 16 bora.

Miamba mingine iliyofuzu kwa hatua hiyo ya 16 bora ni  Inter Milan waliowanyuka Rapid Viena mabao manne kwa bila, Valencia waliopata ushindi wa bao moja kwa bila dhidi ya Glascow Celtic na kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao matatu kwa bila,  huku Benfica ya Ureno wakiwatupa nje Galatasaray ya Uturuki kwa ushindi wa jumla wa mabao mawili kwa moja baada ya matokeo ya suluhu.