Algeria yavuliwa Ubingwa wa Afrika

0
1043

Timu ya Taifa ya Algeria jana wamevuliwa ubingwa baada ya kuchapwa 3-1 na Ivory Coast katika mchezo wa mwisho wa Kundi E wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Douala nchini Cameroon.

Mabao ya Tembo wa Ivory Coast yamefungwa na Franck Kessie dakika ya 22, Ibrahim Sangare dakika ya 39 na Nicolas Pepe dakika ya 54, wakati la Algeria waliotwaa taji hilo mwaka 2019 nchini Misri limefungwa na Sofiane Bendebka dakika ya 73, baada ya nyota wa Manchester City, Riyad Mahrez kukosa penalti dakika ya 60.

Mechi nyingine ya Kundi E, imeshuhudia bao pekee la Pablo Ganet dakika ya 38 likiipa ushindi Equatorial Guinea wa 1-0 dhidi ya Sierra Leone katika mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Limbe.

Ivory Coast inamaliza na pointi saba kileleni, ikifuatiwa na Equatorial Guinea pointi sita na zote zina kwenda 16 Bora, wakati Sierra Leone iliyomaliza na pointi mbili na Algeria pointi moja safari inaishia hapo.

Mechi za Kundi F, vigogo wengine barani Afrika, Tunisia wametupwa nje baada ya kuchapwa 1-0 na Gambia bao pekee la Abdoulie Jallow dakika ya 90.

Nayo Mali ikaichapa Mauritania 2-0, mabao ya Massadio Haïdara dakika ya pili na Ibrahima Koné kwa penalti dakika y 49 mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Douala.

Mali imemaliza na pointi saba, sawa na Gambia na zote zinakwenda 16 Bora, wakati Tunisia inafuzu kama mmoja wa washindi wa tatu bora kwa kumaliza na pointi tatu na Mauritania iliyomaliza mikono mitupu inaaga mashindano.

Hatua ya 16 Bora itaanza Jumapili kwa Burkina Faso kumenyana na Gabon, Nigeria na Tunisia, Jumatatu ni Guinea na Gambia na Cameroon dhidi ya Comoro.

Januari 25 ni Senegal na Cape Verde na Morocco dhidi ya Malawi, wakati Hatua hiyo ya 16 itakamilishwa Januari 26 kwa mechi mbili ambapo Ivory Coast na Misri zitakua dimbani na Mali dhidi ya Equatorial Guinea.