AL Ahly tunamwondoa – Ahmed Ally

0
749

Msemaji wa Timu ya Simba, Ahmed Ally, amewahimiza wanachama na wapenzi wa timu hiyo kuhakikisha wananunua tiketi zao mapema ili Machi 29, 2024 wajitokeze kwa wingi kwa Mkapa kushangalia timu yao ambayo amesema ina uwezo wa kuifunga Al- Ahly ya Misri.

Huku akishangiliwa na kupigiwa makofi, Ahmed ametoa maombi hayo alipozungumza na wapenzi na wanachama wa klabu hiyo leo Machi 25, 2024 katika eneo la Mwembeyanga, Temeke.

“Ndugu zangu, mara zote tulipoishia robo ni kwa sababu hatukumia vizuri uwanja wa nyumbani. Safari hii hatutaki kufanya makosa. Hawa Ahly tukiwafunga goli tatu kwa Mkapa, kule Misri hawana uwezo wa kuzirudisha hata kama watamwamsha Farao (kutoka kaburini) awasaidie kucheza,” amesema.

Amewakumbusha wapenzi wa Simba kwamba katika mashindano ya Kombe la Ligi ya Afrika (AFL), Simba walianza kuifunga Ahly kwa Mkapa kabla ya kufanyika makosa na ndipo wakachomoa.

“Kimsingi tulitoka nao droo, hapa Dar na kwao Misri, wao wakaendelea kwa sababu ya kanuni tu. Safari hii tuhakikishe tunawapiga nyingi kwa Mkapa. Kwa hiyo kila mwana-Simba atumie kila alicho nacho; kuja uwanjani kushangilia, kumwomba Mungu na chochote kile atakachoweza kuhakikisha Simba inashinda na kuingia nusu fainali,” amesema.

Wakati akiwahimiza wanachama kuhakikisha wanakata tiketi mapema, amewataka wachezaji kuichukulia mechi itakayopigwa Dar es Salaam kuwa ya kufa na kupona na kwa upande wa viongozi wenzake kuhakikisha kuanzia sasa hawalali ili kuona kila kitu kinakwenda sawa.