MAMBO YA KUZINGATIA KABLA YA KUANZA SAFARI

0
2716

Wahenga wanasema safari ni hatua, kauli inayomtaka kila mtu kufahamu kuwa safari inahitaji maandalizi.Hivyo ni vema kuweka mazingira sawa ya safari yako kabla hujaianza.

Fahamu yapo mambo mengi ya kuzingatia kabla ya kuanza safari hasa katika kupindi hiki cha sikukuu na mwisho wa mwaka ambapo watu wengi hupenda kusafiri.Na haya ni baadhi tu ya mambo hayo;

Ikiwa ni safari za ndani ya nchi hakikisha umebeba kitambulisho kinachokubalika/ kukutambulisha, na kwa safari za nje ya nchi kagua uhalali wa hati yako ya kusafiri kama ipo ndani ya muda wa matumizi angalau isiwe chini ya miezi sita.

Fahamu vema hali ya hewa ya eneo unalokwenda ili ikusaidie kubeba mahitaji muhimu ya eneo hilo. Ikiwa utatumia usafiri binafsi ni vema kuifahamu kabla barabara utakayoitumia lakini pia kama ni usafiri wa umma ni vema ukafahamu muda wa kuwasili unapokwenda.

Jiwekee mpango wa safari yako ili kusaidia kupata suluhu ya haraka kwa dharura zitakazojitokeza kabla na katikati ya safari. Pia ni vema kufanya maandalizi mapema ya usafiri utakaotumia na mahali utakapofikia.

Hakikisha unapumzika vya kutosha kabla ya kuanza safari yako. Ikiwa utaendesha gari umbali mrefu ni muhimu kupumzika kabla na wakati wa safari.

Beba vitu muhimu katika safari yako. Safari inahitaji maandalizi hivyo vitu kama kadi za benki, vitambulisho, kadi za chanjo, kadi ya bima ya afya na mahitaji mengine binafsi ni vyema yakazingatiwa.

Fahamu tamaduni ya eneo unalokwenda. Hii itakusaidia kujua namna ya kuishi, na hata mavazi yanayoendana na eneo hilo. Vilevile itasaidia kufahamu namna jamii hiyo huishi na hivyo kukupunguzia usumbufu.

Kagua na fanya maandalizi ya gari lako ikiwa utatumia usafiri binafsi, na hiyo ni pamoja kujihakikishia ubora wa magurudumu kama yatahimili safari na hakikisha umebeba vifaa vya dharura kwa ajili ya gari lako.

Usitumie kilevi kabla na wakati wa safari. Hata ikiwa utatumia usafiri wa umma epuka kutumia kilevi ili kuepuka hali ya kushindwa kujizua kusababisha kero kwa wengine na ikiwa utatumia usafiri binafsi itakusaidia kuwa na akili timamu wakati wa kuendesha gari, na hivyo kuepuka ajali zinazotokana na uzembe.

Burudani wakati wa safari ni jambo jema, hivyo ikiwa unaweza kubeba muziki utakuweka katika hali nzuri wewe pamoja na wale unaosafiri nao.

Kwa kuwa safari ni hatua pamoja na kufanya maandalizi hayo yote kibinadamu ni muhimu kumuomba Mwenyezi Mungu kwa kusali na kufanya dua 🤲🏼 ili safari yako ikawe na heri.