Mwaka 2023, pato halisi la Taifa lilifikia shilingi Trilioni 148.4 kutoka shilingi Trilioni 141.2 mwaka 2022, sawa na ukuaji wa asilimia 5.1 ikilinganishwa na asimilia 4.7 mwaka 2022.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo wakati akiwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/25 kuelekea kusomwa kwa bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha.
Amesema ukuaji huo ulichangiwa na jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ikiwemo mikakati ya kukabiliana na athari za vita kati ya Ukraine na Urusi pamoja na uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya nishati, maji, afya, elimu na usafirishaji; kuongezeka kwa uzalishaji wa madini, hususan dhahabu na makaa ya
mawe; na kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi iliyochachua shughuli za kiuchumi.
Hata hivyo amesema kiwango cha ukuaji wa Pato la Taifa kwa mwaka 2023 cha asilimia 5.1 kipo chini ya lengo la mwaka la asilimia 5.2.