Zoezi la kutafuta miili ya watu wanaodhaniwa kufa maji baada ya mitumbwi miwili kuzama katika eneo la Mchigondo wilayani Bunda mkoa wa Mara linaendelea, huku ndugu na jamaa wa watu hao wakiiomba Serikali kuongeza nguvu katika zoezi hilo.
Ndugu hao wamesema zoezi la uokoaji bado haliridhishi, kutokana na vifaa vinavyotumika kuwa duni.
Wamesema licha ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kufika eneo la tukio, bado linashindwa kufanya kazi kwa ufanisi na hivyo mitumbwi kuendelea kuwa njia pekee inayotegemewa.
Kwa siku ya leo hakuna mtu aliyeokolewa akiwa hai wala mwili ulioopolewa.
Mkuu wa wilaya ya Bunda Dkt. Vicent Anney amesema watu 14 waliokolewa wakiwa hai hapo jana baada ya ajali hiyo kutokea na 12 ndio wanaodhaniwa kufa maji.
Amesema zoezi la uokoaji linakwamishwa na uwepo wa upepo mkali unaosababisha wimbi pamoja na kuongezeka kwa tope.