Vijana wanaofanya zoezi la kuopoa miili ya watu waliozama ndani ya Mto Mori katika Kijiji cha Kowak wilayani Rorya mkoani Mara kufuatia kuzama kwa mtumbwi unaotumika kuvusha watu, wameiomba Serikali kuwasaidia vifaa vya uokozi ili zoezi liende kasi
Vijana hao ambao wanaendelea na uopoaji kwa siku ya pili sasa, wamesema zoezi hilo linakuwa gumu kutokana na njia za asili wanazotumia, hivyo kuisihi Serikali kuagiza watu zaidi wenye utaalamu wa kuogelea pamoja na vifaa ili kuongeza nguvu katika zoezi hilo.
Katika ajali hiyo ambapo mtumbwi ulizama jana ukiwa na watu 10, watano waliokolewa wakiwa hai, huku watano wengine wakizama ambapo tayari miili miwili imeopolewa, mmoja akiwa wa mtoto.
Akizungumzia hali hiyo Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka amesema tayari wataalam wa majini wamekwishaanza zoezi hilo.
Amesema mapema asubuhi kikosi cha wazamiaji walianza zoezi hilo, ambapo walifanikiwa kupata mwili mmoja ambao haujajulikana kama ni miongoni mwa wanaotafutwa au la.
Amewataka Wananchi kuendelea kuwa na subira wakati zoezi hilo likiendelea.