Ziara ya kwanza ya Jokate Temeke, atoa maagizo

0
429

Mkuu wa wilaya ya Temeke mkoani Dar es salaam Jokate Mwegelo amefanya ziara ya kwanza wilayani humo tangu aapishwe kushika wadhifa huo, na kutoa maagizo matatu kwa mkandarasi anayejenga barabara ya mwendokasi kutoka Gerezani mpaka Mbagala Rangi Tatu.

Ziara hiyo imemfikisha katika makutano ya barabara ya Kilwa na Morogoro eneo la Uhasibu, na kumtaka mkandarasi anayejenga mradi huo kuhakikisha anaweka mazingira mazuri ya magari kupita wakati ujenzi ukiendelea.

Agizo la pili kwa Mkandarasi huyo ni kuhakikisha anakarabati njia za pembeni ya mradi huo, ili kufanya magari yanayotumia barabara hiyo kutembea na kuondosha msongamano unajitokeza katika baadhi ya maeneo.

Pia amemuagiza Mkandarasi pamoja na Msimamizi wa mradi huo kuweka mazingira mazuri ya magari kupita katika barabara hiyo wakati wa maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam yanayotarajiwa kuanza tarehe 28 mwezi huu.

Baada ya kutoa maelekezo hayo, Jokate amewahakikishia Wananchi wa Temeke kuwa yupo tayari kushirikiana nao katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na kusimamia miradi mikubwa iliyopo katika wilaya hiyo.