Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amefungua Skuli ya Sekondari Mwanakwereke, ambayo hivi sasa inatambulika kwa jina la Skuli ya Sekondari ya Dkt. John Pombe Magufuli.
Katika ufunguzi huo, Dkt. Shein amesema katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wa awamu ya saba jumla ya skuli 26 za sekondari za ghorofa zimejengwa nchini kote.
Aidha, Dkt. Shein kwa niaba ya ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Magufuli, alikubali ombi la uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na kubariki skuli hiyo kuitwa jina la kiongozi huyo pamoja na kukubali skuli ya Sekondari Wingwi kuitwa jina lake.
Shein amesema skuli hiyo iliyojengwa kupitia mradi wa Zanzibar Improving Students Prospects (ZISP) umegharamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia mkopo wa Benki ya Dunia kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 2.6 hadi kukamilika kwake.
Ameongeza kuwa lengo la mradi huo ni kuimarisha ubora wa elimu katika masomo ya sayansi na hisabati ngazi ya sekondari na kuwapatia mafunzo ya somo la kiingereza walimu wote wanaosomesha masomo ya sayansi.
Katika hatua nyengine, Dk. Shein alipinga hoja zinazotolewa na baadhi ya watu kuwa kiwango cha elimu kimeshuka nchini, na badala yake akasema kumekuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaofaulu vizuri katika masomo yao, sambamba na kufahamu kuzungumza lugha za kigeni, hususani Kiingereza.
“Kipimo cha elimu Zanzibar hakijashuka, kuna wanafunzi wapatao 124 wa kidato cha sita ambao wamepata Divisheni ya kwanza, huku divisheni ya nne ikipungua na divisheni zero kufutika kabisa,” alieleza.
Katika hafla hiyo viongozi mbali mbali wa kitaifa walihudhuria akiwemo mgombea wa kiti cha urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dkt. Hussein Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdallah Sadalla, mawaziri pamoja na wanafunzi.