Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imedhamiria kuondoa vitendo vyote vya unyanyasaji wa Wanawake vinavyoendelea kukithiri katika maeneo mbalimbali.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui wakati wa maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani kwa upande wa Zanzibar, mgeni rasmi akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Amesema vitendo vya udhalilishaji kwa Wanawake na Watoto wa kike umekuwa ukiitia doa Zanzibar, hivyo Serikali haitakubali jambo hilo liendelee.
Kwa mujibu wa Waziri Nassor Ahmed Mazrui, wale wote wanaoendeleza vitendo vya udhalilishaji wa Wanawake Zanzibar watafikishwa katika vyombo husika pindi watakapobainika.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Dunia kwa mwaka huu upande wa Zanzibar ni zingatia usawa wa kijinsia kukabiliana na mabadiiliko ya Tabianchi kwa maisha endelevu.