Zaidi ya watumishi 12,000 wa afya kuajiriwa

0
327

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kuwa inakusudia kuajiri watumishi wa afya 12,476 katika mwaka wa fedha 2020/21 ili kukabiliana na changamoto ya upungufu uliopo nchini.

Ahadi hiyo imetolewa leo bungeni, Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Mwantumu Zodo ambaye alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na upungufu wa watumishi wapatao 16,000 hapa nchini.

Dkt. Mollel amesema Serikali inatambua upungufu wa watumishi katika sekta ya afya ambapo kwa kiasi kikubwa umechangiwa na mahitaji mapya yanayotokana na ujenzi wa hospitali mpya na upanuzi wa hospitali za rufaa za kanda, mikoa, halmashauri, vituo vya afya na zahanati.

“Serikali inachukua hatua mbalimbali kukabiliana na upungufu wa watumishi ambapo katika kipindi cha miaka mitano (2015-2020) serikali iliajiri watumishi wapatao 14,479, na zaidi ya watumishi 565 walipatiwa ajira za mkataba kwa kugharamiwa na makusanyo ya vituo vya kutolea huduma za afya,” ameeleza Dkt. Mollel.

Aidha, akijibu swali la nyongeza la mbunge huyo, Dkt. Mollel ameongeza kuwa serikali inalifanyia kazi suala la baadhi ya watumishi wasio waaminifu ambao muda wa kuwa eneo la kazi, wao wanakwenda kufanya kazi vituo binafsi na hivyo kudhorotesha utendaji kazi kwenye vituo vya umma.