Septemba 28 kila mwaka dunia inaadhimisha siku ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa.
Kwa mwaka huu wa 2022 kauli mbiu ya maadhimisho hayo inasema ‘kichaa cha mbwa: afya moja, vifo sifuri’, ambayo inaangazia uhusiano wa mazingira, watu na wanyama.
Kitaifa maadhimisho ya siku ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa yanafanyika mkoani Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine itatolewa chanjo bure kwa mbwa na paka na mafunzo ya aina mbalimbali ya namna ya kuwatunza wanyama hao.
Katika kuadhimisha siku ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa duniani, Mganga Mkuu daraja la kwanza wa mifugo kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Justine Asenga amesema hatari ya ugonjwa huo inaweza kuepukika kama mambo kadhaa yatazingatiwa.
Ameyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na wafugaji wa mbwa kuwachanja mbwa wao, watu kuepuka kuchokoza mbwa na mbwa awe na mmiliki au afungwe katika sehemu maalum ya matunzo.
Akizungumza katika na mahojiano kwenye kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa mbashara na TBC, Dkt. Asenga pia ameweka wazi kuwa kisheria mfugaji wa mbwa hatakiwi kumwacha mbwa wake azurure, hivyo ni muhimu mfugaji azingatie ufugaji bora wa mbwa kwa kumpatia huduma za msingi kama chanjo, malazi, kuogeshwa na chakula ili kuepuka maambukizi ya kichaa cha mbwa.
Je, ni kwa kiasi gani tatizo la kichaa cha mbwa lipo Tanzania?.
Mganga Mkuu daraja la kwanza wa mifugo kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Justine Asenga amesema hapa nchini ugonjwa wa kichaa cha mbwa upo na ni hatari kutokana na aina ya virusi vinavyosambaza ugonjwa huo.
Virusi vya kichaa cha mbwa husababisha maambukizi ya kichaa cha mbwa ambapo huenea kupitia mate ya wanyama walioambukizwa.
Wanyama walioambukizwa wanaweza kueneza virusi kwa kuuma mnyama mwingine au binadamu, na kwa nadra kichaa cha mbwa kinaweza kuenea wakati mate yaliyoambukizwa yanapoingia kwenye sehemu ya wazi kama vile mdomo au macho.
“Virusi hivi huambukiza wanyama wote wenye damu joto, madhara yake ni kifo na huwa hauna tiba bali chanjo ya kuzuIa ugonjwa huu.” amesisitiza Dkt. Asenga
Dalili za kwanza za kichaa cha mbwa ni zipi?.
Dkt. Asenga amefafanua kuwa dalili za kichaa cha mbwa zinaweza kuwa sawa na za mafua na zinaweza kudumu kwa siku mfululizo. Lakini dalili za baadaye zinaweza kujumuisha homa, maumivu ya kichwa, kichefuchefu na kutapika, wasiwasi na mawazo, mkanganyiko, kuhangaika kupita kiasi, ugumu wa kumeza, kutoa mate kupita kiasi, hofu inayoletwa na majaribio ya kunywa maji kwa sababu ya ugumu wa kumeza maji, kukosa usingizi na kupooza kwa baadhi ya sehemu za mwili.
“Ni muhimu kwa mtu kupata matibabu ya haraka yanayotolewa na wataalamu wa afya ikiwa umeng’atwa na mnyama yeyote au ukikabiliwa na mnyama anayeshukiwa kuwa na kichaa cha mbwa, pia Tanzania inajitosheleza tuna vifaa vya maabara na vitendeakazi vya kupima sampuli za kichaa cha mbwa.” ameeleza Dkt. Asenga